YANGA YASHUSHA STRAIKA WA AFCON


HUENDA Yanga wakatimiza ahadi yao ya kutangaza ubingwa mapema msimu ujao, hii ni kutokana na usajili wa nguvu wanaoufanya, kwani baada ya kunasa saini ya baadhi ya wachezaji muhimu, sasa wameelekeza nguvu zao nchini Ivory Coast na muda wowote watashusha mtambo wa mabao.
Straika huyo, ambaye wanamuwinda kwa udi na uvumba, ni Aristide Bance, ambaye amekipiga katika timu mbalimbali barani Ulaya, ikiwamo Ujerumani pamoja na Afrika.
Kwa sasa straika huyo anaichezea timu ya Asec Mimosas ya nchini kwao Ivory Coast, lakini ameshawahi kupita nchini Uturuki akiichezea Samsunspor, pia 1. FSV Mainz 05 ya nchini Ujerumani.
Straika huyo ambaye kucheka na nyavu ni jambo la kawaida kwake, pia aliichezea Chipa ya nchini Afrika Kusini katika msimu wa 2015/16, akiifungia jumla ya mabao matatu katika michezo 14 aliyocheza.
Kwa ujumla straika huyo mpaka sasa amepitia timu 19, lakini mafanikio yake makubwa aliyapata kwenye soka la Ujerumani pamoja na Ubelgiji, ambapo timu alizozichezea alifunga idadi kubwa ya mabao kuliko kwingine alikopita.
Akiwa nchini Ujerumani na 1.FSV Mainz 05, alifunga jumla ya mabao 24 katika michezo 62 aliyocheza, huku idadi yake kubwa zaidi ya mabao ikiwa ni nchini Ubelgiji, akiwa na timu ya Loreken, akifunga jumla ya mabao 27 katika michezo 77 aliyocheza msimu wa 2003-2006.
Shabiki wa kawaida anaweza akajiuliza swali kwamba, kama alishawahi kupita timu hizo kubwa, Yanga wanawezaje kumudu dau lake? Jibu ni jepesi sana, kwani hiyo timu anayoichezea kwa sasa inamlipa shilingi za Tanzania milioni 4.
Fedha hiyo ni ndogo sana kwa jeuri waliyonayo Yanga, kwani hata hao akina Donald Ngoma wanalipwa zaidi ya hivyo, hivyo hiyo si ishu kabisa kwa vigogo wa mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kigogo mmoja wa Yanga ameliambia DIMBA kwamba, mipango inasukwa ya chini kwa chini ili kukamilisha dili hilo, ambapo kama likitiki itakuwa ni bahati mbaya kwa Justice Zullu ‘Mkata Umeme’, kwani mkataba wake unaweza kupigwa stop.
“Tumemuangalia namna ya uchezaji wake tukagundua anatufaa na jambo la kufurahisha ni kwamba amepitia nchi nyingi, ikiwamo Ujerumani, hiyo ikimaanisha kuwa ni mzoefu wa siku nyingi. Kuhusu dau hilo halina shida, kwani hata hapo alipo fedha anayolipwa haikuti ile ya Ngoma (Donald),” alisema kigogo huyo.

Comments


Popular posts from this blog

ILE SINTOFAHAMU YA NANI BINGWA WA VPL HII HAPA

Michezo:Ajibu huyo yanga

ELIZABETH MICHAEL ' LULU' awafungukia wasanii wa bongo move

fahamu kilichojiri nyumbani kwa Tundulisu