Mnyika awaponza askari sita, kamanda asema jeshi linawahita.
Dodoma. Mbunge wa Kibamba (Chadema), John Mnyika amewaponza askari sita waliokuwa zamu ya kulinda ndani ya ukumbi wa Bunge baada ya Spika Job Ndugai kuamuru wahamishwe vituo vya kazi na kupelekwa wilayani.
Hatua hiyo imekuja kwa kile kilichoelezwa na spika kuwa askari hao walishindwa kutekeleza sawasawa amri ya kumtoa Mnyika ndani ya ukumbi huo.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa alisema kama Bunge haliwahitaji askari hao, jeshi hilo linawahitaji na watapelekwa katika wilaya nyingine.
Sakata hilo lilijitokeza Ijumaa wiki iliyopita wakati Mnyika alipokuwa akipinga kuitwa mwizi na mmoja wa wabunge alipokuwa akichangia hotuba ya bajeti ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2017/18.
Ndugai alimtaka Mnyika kutohudhuria vikao vitano vya Bunge na adhabu inamalizika Ijumaa wiki hii.
Habari za kuhamishwa kwa askari hao zilianza kusambaa mkoani hapa juzi na kuthibitishwa na Spika Ndugai jana wakati wabunge wakichangia mapendekezo ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge iliposoma hukumu ya wabunge wawili wa Chadema.
Halima Mdee (Kawe-Chadema) na Ester Bulaya (Bunda-Chadema) waliadhibiwa baada ya kudaiwa kudharau mamlaka ya spika.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana mjini hapa, askari hao waliopangwa zamu siku hiyo wametawanywa katika wilaya mbalimbali zilizopo mkoani hapa mbali na Wilaya ya Dodoma.
Baada ya kuondolewa kwa askari hao, askari waliolinda usalama ndani ya Bunge jana ni waliokuwa wakilinda katika milango ya kuingilia bungeni.
“Hawawezi kuwachukua nje ya maeneo ya Bunge kwa sasa kwa sababu askari wanaohudumia humu ndani wamepata mafunzo maalumu juu ya kazi hiyo,” alisema mmoja wa askari mkoani hapa.
Akizungumza bungeni jana, Ndugai alisema amekiondoa kikosi cha askari hao kwa kuwa hakikutimiza wajibu wao vizuri.
Akirekebisha kauli ya mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea, alisema Mnyika ambaye pia ni waziri kivuli wa Nishati na Madini aliondolewa ndani ya ukumbi huo kama mwizi. “Naomba kwanza nirekebishe aliyoyasema mheshimiwa Kubenea, kuhusu mheshimiwa Mnyika kutolewa kama mwizi, si kweli. Askari wale walimtendea utu ambao haujawahi kuonekana mpaka nikawa nawashangaa ni askari au sio,” alisema Ndugai.
“Kwa sababu hiyo kwa kutokutimiza wajibu wake sawasawa kile kikosi kimehamishwa chote, hakipo hapa. Askari watakaokuwapo hapa ni wale ambao wakiambiwa wanatekeleza.”
Alisema mbunge akiambiwa afanye kitu anatakiwa afanye kiheshimiwa.
“Hivi anafanya kiheshimiwa? Ukivua uheshimiwa wako sasa utakuwa umeamua kuwa kitu kingine na utakuwa treated (tendewa) na askari kadri walivyofundishwa. Kwa kadri unavyouondoa uheshimiwa wako ndivyo watakavyofanya. Na tutaendelea kuvibadilisha vikosi hivyo mpaka tupate kile chenyewe,” alisema.
Ndugai ambaye pia ni mbunge wa Kongwa alisema mabadiliko ya vikosi vya askari wa Bunge yatafanyika kila wakati ili wapatikane askari watakaoweza kuwaondoa wabunge wakorofi kwa staili anayotaka spika.
Akizungumzia hatua hiyo, Mambosasa alisema askari sita waliokuwapo bungeni ndio waliohamishwa na kupangiwa vituo vya kazi katika wilaya nyingine.
Mnyika hakuweza kupatikana kuzungumzia suala hili kutokana na kuwapo mjini Moshi kwenye shughuli za kuuaga mwili wa mwasisi wa Chadema, Philemon Ndesamburo.

Comments