Kasi ya Rais Magufuli kama mtego wa panya kwa Takukuru

Katika kipindi cha miezi sita iliyopita, Rais John Magufuli ameshatoa maagizo mengi yanayohitaji uchunguzi huku akisema bado anawaona watuhumiwa wa rushwa mtaani lakini hawakamatwi.
Wachambuzi waliozungumza na gazeti hili wanasema, kasi hiyo anayohitaji Rais ni mtego kwa uongozi wa taasisi hiyo ambayo inatakiwa kufanya kazi kwa weledi zaidi badala ya kukidhi tu mahitaji na malengo ya kisiasa. Wengine wanasema haraka hiyo inayotakiwa, isipoangalia sheria na weledi itaathiri shughuli za kiuchunguzi kwa watuhumiwa hao wa ufisadi.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Valentino Mlowola aliyethibitishwa kuwa mtendaji mkuu wa taasisi hiyo Januari 26, mwaka jana, anasema kasi anayohitaji Rais haiwezi kuathiri utekelezaji wa shughuli za kiuchunguzi kwa kuwa rasilimali na nguvu ya kutosha iliyopo inajitosheleza.
Mlowola anasema kinachofanyika kwa sasa ni kuhakikisha kasi hiyo ya Rais inaenda sanjari na utekelezaji wa sheria.
Anasema, anachosema Rais ni matamanio ya Watanzania wengi kuona haki ikitendeka mapema kwa watuhumiwa.
“Hata mtuhumiwa ana haki yake, hata wewe ungetamani kuona haki ikipatikana haraka kwa hiyo hakuna agizo lisilotekelezwa katika hayo ya Rais na tunayafanyia kazi,” anasema mkuu huyo.
Kuanzia Aprili hadi Septemba mwaka huu tayari Rais Magufuli ameeleza mara kadhaa kukatishwa tamaa na kasi ya kushughulikia wahusika ambao alidai wengine anawaona lakini hawakamatwi.
Septemba 7, mwaka huu Rais Magufuli alipopokea ripoti za uchunguzi wa madini ya Tanzanite na almasi kutoka kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, aliikabidhi palepale kwa Mlowola na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kwa ajili ya kufanyiwa kazi mara moja.
Agosti 28, mwaka huu, Rais Magufuli aliwataka viongozi wa Takukuru kutokuwa na kigugumizi cha kuchukua hatua pale wanapokuwa na ushahidi dhidi ya watu wanaojihusisha na vitendo vya rushwa.
“Kuna mambo mengi ya hovyo yanafanyika, tumehakiki pembejeo za ruzuku na kubaini madai ya Sh48 bilioni ni hewa, tumebaini wafanyakazi hewa zaidi ya 19,500, tumebaini kaya maskini 56,000 hewa zilizopaswa kupata fedha Tasaf, tumebaini wanafunzi hewa 5,850 waliotakiwa kupata mkopo, kuna vichwa vya treni 11 vimeletwa bila kuwapo mkataba na mengine mengi. Haya yote yanafanyika kwa rushwa, nataka kuwaona mnachukua hatua stahiki,” aliagiza.
Siku tatu kabla ya maagizo hayo, Rais Magufuli alipomuapisha Brigedia Jenerali John Mbungo kuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, aliagiza taasisi hiyo pia kufanya kazi bila hofu ili Tanzania iwe nchi isiyo na rushwa hali itakayoharakisha maendeleo kuwafikia wananchi wa kawaida.
Alisema yeye kama kiongozi atapambana na tatizo hili huku akiomba ushirikiano kutoka kwa wananchi
Mbali na maagizo hayo, Rais pia amekuwa akichukua hatua mara moja pake anapopata taarifa zinazowahusisha wateule wake na masuala ya ufisadi.
Alipopokea ripoti ya uchunguzi wa makinikia, Mei 24, mwaka huu, alitengua nafasi ya waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo huku akiagiza taasisi hiyo kuanza uchunguzi kwa watendaji wote wa Wakala wa Ukaguzi wa Madini nchini (TMAA) ili hatua za kisheria zichukuliwe.
Maagizo mengine aliyatoa Aprili 12, mwaka huu, alipokuwa akipokea ripoti ya mwaka 2015/2016 ya utendaji kazi wa Takukuru alilaani mazingira ya mtuhumiwa kukamatwa lakini ushahidi ukafichwa au kutopelekwa mahakamani, matokeo yake rushwa inaendelea na wahusika wanabaki salama.
Mbali na uchunguzi ulioagizwa na Rais, yapo matukio mengine makubwa yanafanyiwa uchunguzi likiwamo suala la Lugumi kuhusu mradi wa ufungaji wa vifaa vya mawasiliano na mengine.
Nyingine ni sakata la kampuni ya mafuta kukwepa kodi, ununuzi wa mabehewa feki na ukiukwaji wa taratibu za kuwapata wazabuni na matumizi mabaya ya fedha katika Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) na tuhuma mbalimbali zinazowakabili waliokuwa vigogo wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Maoni ya wasomi
Akizungumzia maagizo hayo na utekelezaji wake, Wakili wa Kujitegemea Onesmo Mpinzile anasema kasi anayoitaka Rais Magufuli inaweza kuathiri utendaji au kuongeza kasi katika uchunguzi unaofanyika.
Mpinzile anasema taasisi hiyo inafanya kazi za kiuchunguzi katika makosa ya jinai kwa kuzingatia sheria ili kujiridhisha endapo mtuhumiwa ana kosa la kufikishwa mahakamani.
“Kwa hiyo kutofautiana na kasi ile anayotaka Rais kwa watu anaowaona, lakini hawakamatwi inaweza kuwa ni umakini na weledi wa hali wa Takukuru, inataka ijiridhishe kwanza pasipo na kuacha shaka,” anasema.
Mwanasheria huyo ambaye amewahi kushughulikia kesi za makosa ya jinai, anasema kesi nyingi zinazopelekwa mahakamani zinakuwa hazijakamilisha upelelezi wake hatua inayoathiri uendeshaji wa kesi na baadhi ya majaji huzifuta.
Hata hivyo, Mpinzile anasema inawezekana pia kasi ya utendaji wa vyombo vya uchunguzi ikawa ndogo kutokana na changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa zikielezwa na taasisi hiyo ikiwamo uhaba wa watendaji na aina ya ushahidi unaohitajika kupatikana katika mazingira magumu ikiwamo njia ya teknolojia ya kisasa.
“Unajua rais anawajibika kwa wapiga kura wake, anataka baadaye aje kuwaeleza Watanzania kwamba, tumekamata na kufunga watu hawa kwa sababu ya rushwa. Takukuru iko chini ofisi ya Rais, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Mkurugenzi wa Upelelezi wa makosa ya Jinai (DCI) na Takukuru wanafanya kazi pamoja lakini tatizo ni vyanzo vingine anavyotumia Rais Magufuli kupata taarifa. Ofisi ya Mwanasheria Mkuu inatakiwa kumshauri Rais kuhusu umakini wa Takukuru,” anasema.
Hata hivyo, kutokana na ugumu wa kasi hiyo, Aprili mwaka jana mbele ya kikao cha makamanda wa polisi wa mikoa, mawakili wafawidhi wa Serikali na wakuu wa upelelezi wa mikoa na vikosi, Rais Magufuli aliwashutumu baadhi ya mawakili hao kuhujumu kesi za Serikali, kuwa wakati mwingine wanashirikiana na mawakili wa watuhumiwa, na hivyo Serikali kushindwa kesi.
Mhadhiri kutoka Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala bora, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM), Richard Mbunda anasema ni jambo jema Rais kuisukuma Takukuru katika utekelezaji wa majukumu yake lakini taasisi hiyo haitakiwi kutumika kisiasa katika utendaji wake.
“Takukuru ipewe nafasi ya kujiridhisha kwa ushahidi wa kutosha, ifanye kazi kwa weledi ili kuepuka kesi zisizokuwa na ushahidi, tumeona watu wakikamatwa bila ushahidi na matokeo yake Serikali inashindwa, badala yake inadaiwa fidia. Tuepuke kushusha maksi katika utawala kwa kukamata bila ushahidi wa kutosha,” anasema Mbunda.
Na mwananchi

Comments


Popular posts from this blog

Silole aweka wazi mambo

Diego Costa na Antonio Conte, ndani ya vita nzito

Waziri Mkuu Mstaafu, Fredrick Sumaye ameitaka Serikali ya awamu ya tano kukivumilia

KENYA :Caroline Odinga akutwa amekufa

WANAWAKE WEUSI WENYE NGUVU YA PESA DUNIANI.

Ujumbe wa Idris Sultan kwa Zari