Polisi Wilaya ya Arusha imepiga marufuku mikutano ya hadhara ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema kwa maelezo kuwa kutakuwa na ujio wa viongozi wa kitaifa jijini hapa. Pia, kuzuiwa mikutano ya mbunge huyo wa Chadema kunahusishwa na tukio la kuungua moto nyumba za polisi. Katika barua ya Mkuu wa Polisi Wilaya ya Arusha, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi SSP E.Tille kwenda wa Lema Jumatano, imeeleza mikutano yake imesitishwa. Mikutano hiyo ilikuwa ifanyike leo Alhamisi na kesho. Katika barua hiyo, Jeshi la Polisi limeeleza kuwa tarehe ambazo mikutano hiyo, imepangwa zina mwingiliano na ratiba za shughuli za kiserikali za viongozi wa juu wa Serikali inayoishia Oktoba 4. Pia, amesema janga la moto katika kambi ya polisi lililotokea jana usiku limeleta madhara makubwa hivyo, nguvu kubwa itaelekewa huko. "Unashauriwa kupanga mikutano yako tarehe yoyote kuanzia Oktoba 5, 2017 pia rejea mazungumzo yangu na wewe ofisini kwangu ya tarehe 29/09/2017," inasomeka barua hiyo. Hat...